https://grain.org/e/7155

SIMAMISHA MAKUBALIANO YA BIASHARA HURIA BARANI AFRIKA ​

by bilaterals.org & GRAIN | 27 May 2024


AfCTA: Biashara huria zaidi? Kwa maslahi ya nani?

Kuanzia miaka ya mapema ya 2000, Wafrika walisema "HAPANA KWA EPAs" (Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi – EPA [Kwa Kiingereza]) ambayo yalikuwa yakihimizwa na Ulaya ili kuendeleza unyonyaji wa kikoloni wa Kusini mwa dunia. Sasa, mradi mwingine wa uliberali mamboleo unatishia Bara la Afrika: Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).

Makubaliano haya makubwa ya kibiashara ni mradi wa Umoja wa Afrika (AU), ukifadhiliwa na wadau wakubwa wa kiuchumi kama Marekani, Umoja wa Ulaya, China, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Biashara na Maendeleo Duniani (UNCTAD), Shirika la Kimataifa la Biashara (WTO) na Benki ya Dunia. Makubaliano haya yamelenga kuyaleta pamoja masoko ya Afrika, kuongeza wigo wa biashara ndani ya Afrika na kuboresha ushirikiano wa kikanda. Makubaliano haya yamesainiwa na mataifa 54 kati ya 55 ya Umoja wa Afrika. Wakati makubaliano hayo yaliingiwa mwaka 2019, baadhi ya kanuni/ sheria zake za kibiashara zimeanza kutekelezwa kuanzia 2022 na zimetekelezwa kati ya mataifa saba tu. Makubaliano ya AfCTA yanalenga kuwezesha biashara huria ya bidhaa, miongoni mwa mataifa ya Afrika, kwa asilimia 97. Pia yanalenga kuweka kanuni za kibiashara katika huduma, na katika hati miliki bunifu, uwekezaji na biashara ya kimtandao. Mchakato wa mazungumzo na majadiliano [kuhusiana na Makubaliano haya] umekosa uwazi, ambapo taarifa zinazopatikana ni kupitia nyaraka zilizovujishwa. Biashara Afrika imekuwa ikiendeshwa na wafanyabiashara wadogo, wengi wao wakiwa wanawake, katika namna isiyo rasmi. Makubaliano ya AfCTA inapuuza uhalisia huu, na imejikita katika kuongeza ushindani miongoni mwa makampuni makubwa.

Hivyo basi, makubaliano haya ya kibiashara yana maana gani kwa Muafrika wa kawaida katika wakati wa majanga makubwa ya kimazingira, kiuchumi na chakula?

Msisitizo wa ajenda ya kilimo biashara

Kilimo cha wakulima wadogo na mifumo ya chakula ya Kiafrika iko katika hatari ya kudhohofishwa na AfCTA. Hatari moja kubwa ni kwamba, inaweza kupelekea kuongeza nguvu ya kisheria ya kufanya mbegu za wakulima wadogo kuwa kosa la jinai. Rasimu ya Sheria ya AfCTA ya Hati Miliki Bunifu inasisitiza kuhuisha sheria na kanuni ili “kulinda” aina mbalimbali za mimea, rasilimali jeni na maarifa ya asili. Hii ina maanisha kuyafanya kuwa ni mali binafsi. Hivyo, kampuni za mbegu zitaweza kuwazuia na kuwadhibiti wakulima kutunza na kugawana mbegu zinazolindwa na kutambulika kisheria. Matokeo yake, baio-anuwai – uti wa mgongo wa utamaduni wa chakula cha Muafrika na msingi wa Uhuru wa Chakula – itapotea na nguvu ya viwanda vya kilimo na chakula itaongezeka. Haikubaliki kugawa na kuruhu uhodhi wa haki katika mbegu kwa mtu yeyote yule.

Haki za Wafanyakazi ziko hatiani

Kuhamasisha maendeleo, AfCTA inahimiza uendeshaji wa shughuli katika Maeneo Maalum ya Kiuchumi, ambapo sheria/ kanuni hulegezwa kwa ajili ya kuvutia uwekezaji. Maeneo hayo Maalum ya Kiuchumi yanazipa kampuni likizo za kodi na kuziondolea masharti ya kisheria za kimazingira na sheria nyenginezo. Kwa wafanyakazi, hii inamaanisha mazingira duni ya kazi, ujira mdogo, huduma mbovu kazini, masaa mengi ya kazi, ukatili dhidi ya wanawake na mazuio dhidi ya shughuli za vyama vya wafanyakazi. Maeneo haya Maalum ya Kiuchumi pia yanapelekea katika uporaji na ufukuzwaji katika ardhi, hususani pale ambapo ardhi inabadilishwa kutoka matumizi ya kilimo kuwa matumizi ya viwanda.

Upatikanaji wa madawa uko hatiani

Makubaliano haya yanajumuisha vifungu vya hati miliki bunifu, ambavyo vinaweza kuathiri uingizaji na uzalishaji wa madawa rafiki kwa makampuni ya ndani. Kiambatanishi kuhusiana na leseni bunifu (patents) zitawekwa wakati ujao, lakini mchakato wa majadiliano unatarajiwa kuendelea kubaki kuwa wa siri, licha ya kwamba unaweza kuwa na athari nyingi kwa afya ya umma.

Makampuni yanaweza kuishtaki serikali

Makubaliano (ya AfCTA) yaliyovuja yanaonesha kwamba nchi wanachama zinaweza zikatakwa kuanzisha Mifumo ya Utatuzi wa Migogoro kati ya Muwekezaji na Serikali (ISDS). Mfumo huu wa haki, utakaotambulika na mfumo wa haki uliopo, utaruhusu wawekezaji kutoka nje kuishtaki serikali katika Mahakama za Uamuzi, endapo sheria au kanuni mpya zinaathiri uwekezaji wao au matumaini yao ya faida. Mifumo hii ya Utatuzi wa Migogoro imekosolewa duniani kote kwa kuruhusu wawekezaji kubadili sera za umma za mataifa huru na yenye mamlaka kamili. Pia, imepelekea kwa adhabu kali, ambapo mabilioni ya dola yamelazimika kulipwa na umma. Serikali za Kiafrika zimepoteza kesi nyingi kati ya kesi 99, za ISDS, zilizofunguliwa dhidi yao mpaka sasa, chini ya mikataba ya uwekezaji kati ya nchi mbili.

Sheria ya Biashara ya Kidijitali iko katika mazungumzo ndani ya AfCTA, lakini yanayojadiliwa/ kuzungumza hayako hadharani. Ni dhahiri kwamba sheria hii itasaidia mpango wa Umoja wa Afrika kuanzisha soko moja la kidijitali barani. Hii inamaanisha kuondoa 'vikwazo' vya kisheria na kiufundi kwa biashara, kama vile hatua zilizotumiwa na nchi za Afrika katika kulinda faragha. Kwa mfano, inaweza kupiga marufuku mahitaji ya mahali husika yanayozuia taarifa nyeti, kama zinazohusiana na taarifa binafsi za afya, kutochakatwa nje ya nchi ya mhusika. Ikiwa theluthi tu ya Waafrika wanatumia mtandao mara kwa mara, haijulikani ni nani atakayenufaika na uhuria wa biashara ya kidijitali na biashara mtandaoni.

Madeni zaidi katika miundombinu

AfCTA ni moja ya miradi ya kipekee/ mikuu ya Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika (AU), ambayo inalenga kujenga miundombinu ya ndani ya Afrika. Itahamasisha miradi mikubwa ambayo inakidhi mahitaji ya dola na ya wadau wa kibiashara, kama shoroba ya Nacala, ambayo itakuwa kiungio kati ya nchi ya Msumbiji, Malawi na Zambia, ambapo kwa pamoja itakuwa na barabara na reli yenye urefu wa kilomita 1700. Miradi hii mikubwa hunufaisha zaidi makampuni ya kimataifa na wakati huo huo huzalisha zaidi madeni kwa nchi ambazo miradi hiyo hujengwa. Wakati maendeleo ya miundombinu ni muhimu, yanapaswa yawe kwa maslahi ya umma na yasipelekee katika ongezeko [maradufu] na deni la taifa. Kukumbushia, deni la nje kwa nchi za Kiafrika, mnamo 2022, lilifika bilioni 44 za Kimarekani.

HAPANA kwa AfCTA!

AfCTA imejengwa kutokana na misingi ya Ubepari wa Soko Huria. Inasisitiza mfumo wa “maendeleo” ulioelekezwa katika kuongezeka kwa biashara na uwekezaji, chini ya hadaa ya Umajumui wa Afrika. Hata hivyo, ni kanuni za biashara “sawa sawa” na zile tunazoziona katika WTO (Shirika la Biashara Duniani) na Mikataba Baina ya Nchi Mbili. Hivyo basi, AfCTA inatazamiwa zaidi kuwanufaisha zaidi Watawala wa Kiafrika na Mitaji ya Kimataifa, kwa/ dhidi ya gharama ya jamii za ndani


Kwa taarifa zaidi:
Author: bilaterals.org & GRAIN
Links in this article:
  • [1] https://bilaterals.org/afcfta-287
  • [2] https://grain.org/system/attachments/sources/000/006/643/original/Swahili_ACFTA_01.pdf
  • [3] https://iboninternational.org/download/scramble-for-africa-afcfta-campaign-primer/
  • [4] https://isds.bilaterals.org/