https://grain.org/e/7101

Wimbi jipya la uporaji ardhi linaikumba Tanzania

by GRAIN and La Via Campesina Southern and Eastern Africa | 1 Feb 2024


Tanzania ilikuwa mojawapo wa nchi kuu zilizolengwa katika mapambano ya upatikanaji wa ardhi ya kilimo duniani, kufuatia mdororo na anguko la chakula na uchumi mwaka 2008, na [ardhi hiyo ya kilimo] ilipaswa kusaidia kutoa suluhu ya kukosekana kwa usalama wa chakula duniani. Miradi mikubwa ya kilimo, ambayo ndiyo iliyokuwa chaguo na mikakati rafiki kwa wafadhili, makampuni makubwa ya kimataifa, na baadhi ya serikali, hatimaye ilisababisha madhara makubwa zaidi kuliko manufaa kwa kuongeza migogoro ya ardhi na kuharibu/ kuathiri maisha ya watu. Nchini Tanzania, miradi mingi ya aina hii ilishindwa na kuanguka punde [tangu kuanzishwa] na kusababisha maafa kwa wakulima wadogo. Lakini, licha ya taarifa na rekodi hizi za kusikitisha, serikali ya Tanzania inaendelea na duru nyingine ya uwekezaji wa kigeni katika kilimo biashara, kwa kugeuza maelfu na malaki ya hekta za ardhi kuwa mashamba makubwa, ambapo makampuni makubwa yatazalisha mazao ya kuuza nje ya nchi, na wala si kuzalisha kwa ajili ya chakula cha ndani kwa ajili ya watu wake. Wakati China ikiitazama Tanzania kama chanzo chake kipya cha kuzalisha na kusambaza soya, hatua hii inaweza kuchochea wimbi jipya na lengine la unyang’anyi na uporaji wa ardhi, wenye athari kubwa kwa wakulima wadogo wa Tanzania.


Ilipaswa kuwa mwisho wa kilimo biashara kikubwa [large-scale agribusiness] nchini Tanzania. Mapema mwaka 2019, kampuni ya Kilombero Plantation Limited (KPL), pamoja na modeli ya mfano, iliyopigiwa debe sana, ya Southern Agricultural Growth Corridor for Tanzania (SAGCOT), zilifilisika.[1] Licha ya kupokea mamilioni ya dola kutoka benki za maendeleo za kigeni na wawekezaji, mmiliki wa shamba kubwa la mpunga, kampuni ya uwekezaji binafsi yenye makao yake Uingereza, ilishindwa kulipa deni lake na shamba likachukuliwa na wadeni wake. Benki ya NMB ya Tanzania ilitumia miaka miwili ijayo kutafuta mnunuzi, kabla ya serikali kuingilia kati kulichukua/ kulinunua na kisha kulikabidhi jeshi kusimamia shamba hilo.[2]

Shamba la mpunga lenye hekta 5,818 liliwahi kuoneshwa na kukaririwa na G7 na Jukwaa la Kiuchumi la Dunia [World Economic Forum] kama kielelezo na ushuhuda kwamba kilimo biashara kikubwa kinaweza kusukuma ukuaji wa kilimo barani Afrika. Lakini, wakati kampuni ya KPL ikiwa kwenye majanga ya kifedha, hivyo basi nayo ikawa ni kielelezo dhahiri cha jitihada zilizoshindwa na zilizokosa mwelekeo kuongeza uwekezaji wa kigeni katika kilimo, kwa miongo [miaka kumi].

Anguko la kampuni ya Kilombero ilikuwa mojawapo, katika orodha ndefu, ya miradi ya kilimo biashara nchini Tanzania, iliyoanzishwa na kushadadiwa katika programu mbali mbali zilizokuwa zimefadhiliwa, wakati wa Urais wa Jakaya Kikwete (2005-2015).[3] Programu hizi – kuanzia Kilimo Kwanza (2006), kisha SAGCOT (2010), na hatimaye Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa [Big Results Now] (2013) – zililenga kuhakikisha na kuwezesha maeneo makubwa ya ardhi yaweze kufikiwa na makampuni makubwa, chini ya imani na mtazamo kwamba Tanzania itakuwa kitovu na kinara wa uuzaji wa mazao nje ya nchi, itahakikisha usalama wa chakula na muhimu zaidi, italeta ajira, teknolojia, huduma mbali mbali (mafunzo, pembejeo, mashine, nk) pamoja na masoko mapya kwa wakulima wadogo wanaoishi karibu na mashamba. SAGCOT pekee ilidai ingeleta uwekezaji wa sekta binafsi wa dola bilioni 2.1.[4] Lakini baada ya miaka 10, sehemu ndogo sana ya uwekezaji ulioahidiwa ulikuwa umetokea, na, kati ya miradi michache iliyoanza utekelezaji, mingi kati yao ilishindwa, na imeacha urithi wa matatizo yanayopaswa kushughulikiwa kwa jamii zilizoathirika.[5]

Kufikia wakati wa kufilisika kwa kampuni ya Kilombero Plantations, Rais wa wakati huo wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, alikuwa amechoshwa na kukasirishwa na njia iliyotumiwa na mtangulizi wake, na hivyo alikuwa ameanza kutafuta njia mpya. Aliifuta programu ya Matokeo Makubwa Sasa [BRN] na kisha akaanza kuifunga SAGCOT. Serikali yake ilifuta ufadhili wake katika “Mfuko wa Uwezeshaji” (Catalytic Fund) wa SAGCOT, ambao uliundwa kupitia Mkopo wa Benki ya Dunia - ishara wazi ya mabadiliko ya mtazamo.[6] Pia, alianza mchakato wa kufuta hati miliki za makampuni yaliyoshindwa kutumia ardhi kwa ajili ya uzalishaji.[7]

Lakini mwaka 2021, Magufuli alifariki, na mrithi wake, Makamu wa Rais wake, Samia Suluhu Hassan, alibadilisha mwelekeo haraka. Chini ya uongozi wa Waziri wake wa Kilimo, Hussein Bashe, kilimo biashara kikubwa, kwa mara nyingine tena, kikawa kipaumbele cha serikali na milango ikafunguliwa kwa makampuni ya ndani au ya kigeni yanayotaka maeneo makubwa ya ardhi ya kilimo. SAGCOT ilirejea kwenye jukumu lake la msingi, huku ikiwa na majukumu na mamlaka ya ziada ya kuanzisha ushoroba [korido] nchini kote.[8] Mamia ya mamilioni ya dola za umma zilitengwa na kuwekwa katika bajeti ya umwagiliaji wa kilimo kibiashara kikubwa; na katika programu inayodai kuunga mkono ushiriki wa vijana katika kilimo; na vivyo hivyo, maelfu na malaki ya hekta za ardhi nchi nzima zinatayarishwa na kuunganishwa kuwa "mashamba ya mfumo wa vitalu" [block farms] na kisha kutolewa kwa makampuni kwa uzalishaji wa mazao maalum ya kuuza nje.[9]

Ubashiri wa kesho

Msingi mkuu wa jitihada mpya za Rais Samia kugawa ardhi kwa makampuni ya kilimo ni programu inayoitwa Kujenga Kesho Bora [Building a Better Tomorrow – BBT].[10] Katika programu hii, serikali inabaini na kutenga na kisha kusafisha maeneo makubwa ya ardhi na kuyafanya maeneo hayo kuwa ya kilimo kikubwa, kilimo cha umwagiliaji, kinachoitwa “Kilimo cha Mashamba ya Vitalu”, ambapo kikundi cha vijana na wanawake, haswa kutoka miji mikubwa na wahitimu wa vyuo vikuu, wanapewa maeneo madogo kati ya ekari 1 - 10 (0.4-4 ha), wakati jamii vijijini zinapuuzwa na kutengwa. Julai 2023, Rais Samia alitangaza kwamba vijana wote 52,000 waliokuwa wameomba kujiunga na jeshi mwaka huo wangeorodheswa katika programu ya BBT.[11]

Kila shamba kitalu la BBT linapaswa kuzalisha zao maalum kwa kampuni ambayo inashiriki kuwekeza katika shughuli za uendeshaji na utendaji. Kupitia mfumo huu, kampuni itatoa nyenzo na vifaa/ mashine na itanunua mazao yote. Pia [kampuni husika] inaweza kupata hati ya miaka 99 katika sehemu ya eneo la shamba kitalu, kwa ajili ya kujihusisha na kilimo wenyewe. Wakati huohuo, wakulima wa BBT wanapewa hati za miaka 33 hadi 66, na ingawa wanaweza kuhamisha hati hizo kwa mtu mwingine, hawawezi kubadilisha masharti ya mkataba wao. Hivyo, watakuwa chini ya kampuni inayodhibiti na kusimamia shamba, ambayo inapaswa kuwanunulia nyenzo zote na ambayo wanapaswa kuiuzia mazao yote.[12]

Rais Samia amesema kwamba hekta 690,000 zimebainishwa kote nchini tayari kwa ajili ya kufanywa mashamba vitalu, lakini hakuna taarifa yeyote iliyoko wazi na inayopatikana kwa umma kuhusu yalipo haswa maeneo hayo. Januari 2023, serikali ilichapisha wito wa kwanza kwa mapendekezo ya uwekezaji kwa mashamba vitalu yenye jumla ya hekta 65,000 katika mikoa ya Dodoma, Mbeya, Kagera, na Kigoma. Kampuni zilizokuwa na nia zingeweza kuomba ardhi kati ya hekta 400 hadi 8,000 kwenye kila shamba kitalu.

Mwezi Machi 2023, shamba la kwanza la BBT lilifunguliwa rasmi katika wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alieleza kwamba hekta 162 za awali zilitengwa kwa mafunzo ya vijana 812 waliochaguliwa kushiriki katika mradi huo.[13] Licha ya upatikanaji wa ardhi kuwa changamoto kwa jamii za eneo hilo, vijana wengi waliochaguliwa kwa mradi huo sio wa eneo hilo na wana uzoefu mdogo au hawana uzoefu wowote katika kilimo. Shamba hilo la Dodoma linatarajiwa kuongezeka na kutanuliwa hadi hekta 11,453 na litazalisha zabibu kwa ajili ya kiwanda cha usindikaji/ uchakataji wa mvinyo. Hata hivyo, hadi sasa, hakuna kumbukumbu/ taarifa yeyote iliyotolewa kwa umma kuhusu kupatikana kwa mwekezaji.

Picha ya pamoja ya wakulima vijana katika shamba, kitalu cha BBT Dodoma, Tanzania. Machi 25, 2023. [Chanzo: Twitter (X)]
Prudence Lugengo, mtaalamu wa sera wa SAGCOT, anasema ardhi kwa ajili ya shamba lingine la BBT imetengwa katika mikoa ya Katavi na Tabora. Katika awamu hii, shamba hilo la BBT linaelezwa kuwa kubwa mno, kwani shamba kitalu la hekta 120,000 litazalisha ngano kwa ajili ya kampuni ya kilimo ya Tanzania ya MeTL, inayomilikiwa na bilionea wa Kitanzania na mwanasiasa wa zamani Mohammed Dewji. Kwa mujibu wa Lugengo, MeTL itachukua hekta 50,000 kwa ajili ya matumizi yake binafsi na hekta 70,000 zilizobaki zitatengwa chini ya programu ya BBT ya vijana. MeTL hawakutoa majibu kwa maombi yetu ya kuthibitisha makubaliano hayo, na haieleweki ni namba gani Dewji atakavyofadhili mradi huu.[14] Inafaa kukumbuka kwamba miaka michache nyuma, serikali ya Magufuli ilifuta hati kadhaa za maeneo makubwa ya ardhi ya kilimo ya Dewji kwa sababu ya kushindwa kwake kuzitumia ardhi hizo kwa ajili ya uzalishaji.[15]

Pamoja na changamoto zilizotajwa hapo awali, matumaini ya programu pendwa ya BBT yako mashakani mapema mno, ambapo shutuma kuhusu programu hii zinaenea katika kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii, zikieleza kushindwa kwa serikali kutimiza ahadi zake. Mwishoni mwa Januari 2024, barua inayoelezwa kutoka kwa moja wa vijana washiriki wa programu ya BBT ilisambaa na kuenea katika mitandao ya kijamii, ikieleza kwamba serikali imeshindwa kuwagawia kila mtu hekta 5 za mashamba, kama walivyoahidi (kuachana na ahadi ya mwanzo ya kugawa hekta 10 kwa kila mmoja) na pia serikali imeshindwa kujenga na kuweka miundombinu ya umwagiliaji. Badala yake, vijana 260 ambao wamepita katika mafunzo wamepelekwa Chinangali, kwenye shamba la ekari 600, ambapo wanalima pasipokuwa na mfumo wa umwagiliaji na makazi yenye staha, na wanapaswa kuzalisha alizeti kwa mkataba na kampuni, pasipo kuwa na uhakika wa kugawiwa ardhi wao wenyewe.[16]

Mashamba vitalu ni nini?

"Shamba kitalu" ni eneo kubwa la ardhi ya pamoja lililotengwa kwa uzalishaji wa mazao machache au zao moja. Barani Afrika, programu ya "shamba kitalu" inaweza kuwa na sura nyingi, lakini kwa ujumla serikali inahakikisha kuwa ardhi ziko tayari na zinapatikana kwa ajili ya kilimo biashara kikubwa, inaweka miundombinu (kama barabara au umwagiliaji) na kutambua kampuni moja au mbili kuwa wawekezaji wakuu. Kwa kawaida, sehemu ya ardhi italimwa na kununuliwa na kampuni kwa mkataba wa miaka 99 na sehemu nyingine italimwa na wakulima wa kati hadi wadogo ambao lazima wazalishe mazao kwa kampuni chini ya mkataba.

Zambia ilianza programu tangu mwaka 2006 ya kuanzisha "mashamba vitalu " yenye ukubwa wa hekta 100,000 katika kila moja ya mikoa yake 10. Ingawa serikali haikuweza kuvutia "wawekezaji madhubuti," mwaka 2023 ilikuwa na matumaini ya kufufua programu hiyo kupitia mkopo wa Dola za Marekani milioni 300 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu kwenye mashamba hayo[17]. Serikali ya Malawi pia ilizindua programu ya mashamba vitalu mwaka 2020, iliyojumuisha idadi kadhaa ya kile inachokiita "mashamba makuu” [mega farms] zenye takriban hekta 5,000 kila moja. Hata hivyo, nayo imekabiliana na changamoto ya kuvutia uwekezaji mkubwa kutoka kwa sekta binafsi."[18]Eneo jipya la soya kwa China?

Licha ya shangwe ya matumaini iliyopo tangu kuanzishwa kwa programu ya BBT, kuna ushahidi mdogo unaoonesha kuwepo kwa dhamira ya ushiriki wa sekta binafsi. Mtaji mkubwa ambao umetolewa au kuahidiwa hivi sasa ni kutoka serikalini, ambapo imeahidi Dola za Marekani bilioni 1.4 kwa miaka 10 ijayo, na kutoka kwa kundi lile lile la wafadhili waliounga mkono juhudi za uwekezaji wakati wa programu ya SAGCOT. Hizi ni pamoja na Benki ya Dunia (USD milioni 300), Benki ya Maendeleo ya Afrika (USD milioni 100), AGRA (USD milioni 40), Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (USD milioni 60), na USAID (USD milioni 100).[19]

Soya yanaweza kuwa tofauti, na hususani, soya yanayokusudiwa kwa ajili ya China. Kutokana na kukuwa kwa uhasama na Marekani na vita nchini Ukraine, China ina wasiwasi zaidi kuhusu utegemezi wake kwa nchi hizo mbili kwa soya (pamoja na mahindi), na sasa inatazama Afrika kama chanzo mbadala cha usambazaji. Tanzania ni mojawapo ya nchi tatu za Kiafrika ambazo China imezitambua kwa uzalishaji wa soya kwa ajili ya usafirishaji na usambazaji kwake. Mwaka 2020, China ilipitisha hatua/ mpango wa afya ya mimea [pythosanitary] kuruhusu uagizwaji na uingizwaji wa soya kutoka Tanzania na safari ya kwanza ya usafirishaji ilifanyika mwaka uliofuata kwa kusimamiwa na kampuni kubwa kuliko ya biashara ya nafaka ya COFCO.[20] Novemba 2022, Rais Samia alisaini Mkataba wa Kina wa Ubia wa Mashirikiano ya Kimkakati na China, katika ziara Beijing ambapo usafirishaji wa soya ulitajwa kama kipaumbele cha awali na kikosi kazi kiliundwa kwa ajili ya utekelezaji.

Kwa wakati huu, Tanzania inazalisha tani 200,000 tu za soya kwa mwaka – ikiwa ni sehemu ndogo ukilinganisha na kiwango cha uagizaji wa China cha tani milioni 100 kila mwaka, ambapo kiasi kikubwa hutumika kutengeneza chakula cha wanyama na mafuta ya kupikia. Ili kuwa msambazaji/ muuzaji mwenye tija [kwa China] Tanzania inapaswa kuongeza uzalishaji wake maradufu.

Kampuni kubwa ya mbegu ya China, Yuan Longping High-tech Agriculture, imepewa jukumu la kufuatilia fursa hii. Kampuni hii ni sehemu ya kampuni kuu ya CITIC Group, kampuni kubwa kuliko inayomilikiwa na serikali ya China, na tayari inafanya jukumu la muhimu la kuimarisha udhibiti wa China katika uzalishaji wa soya na mahindi nchini Brazil, ambao ni wauzaji na wasambazaji muhimu zaidi kwa China. Baada ya kuingia nchini Brazil mwaka 2017, mapema Longping ikawa mojawapo ya kampuni kubwa za mbegu nchini humo. Hivi sasa Longping inalenga kufanya vivyo hivyo nchini Tanzania, wakati China ikiazimia kuutumia mfumo na modeli ya Brazil barani Afrika.

"Tunataka kuchukua na kuutumia utaalam wa Longping katika mahindi na soya kwa [Tanzania na Ghana]. Huko, hali ya hewa, joto, na jiografia yake inalingana na ile ya Brazil na ni nzuri sana kwa maendeleo ya kilimo. Tunataka kuwa wawezeshaji wa mchakato huu, na tuwafundishe jinsi ya kupanda na kuzalisha nafaka ili hapo baadaye wawe pia wauzaji kwa China," anasema Aldenir Sgarbossa, Rais wa Longping – katika Utendaji nchini Brazil.[21]

Mwaka 2022 na mapema 2023, Longping ilipeleka ujumbe Tanzania ili kupata ushawishi na kuungwa mkono kisiasa na ili kutambua maeneo ya uzalishaji wa soya. Majaribio ya aina mbali mbali za soya kutoka Brazil yanaendelea, pamoja na mahindi chotara na mbegu za mtama, ambazo zitapandwa kwa awamu na kupishana na soya, kama inavyofanyika nchini Brazil. Wakati hizi aina za awali sio GMO, Longping ina aina mbali mbali ya GMO zinazofanyiwa majaribio na zinasubiri idhini ya kuuzwa kibiashara nchini China, na aina mbali mbali za mahindi ya GMO yameshapata idhini ya matumizi ya binadamu.

Longping inasema itawekeza zaidi ya Dola za Marekani 213 milioni (shilingi bilioni 500) katika awamu ya kwanza ya kukuza uzalishaji wa soya kusini mwa Tanzania na pia itawekeza katika kuboresha miundombinu ya kusafirisha nafaka katika bandari ya Dar es Salaam.

Shughuli za kampuni hiyo nchini Tanzania zinaendeshwa kupitia ubia na mfanyabiashara wa Kitanzania, mfanyabiashara maarufu wa tasnia vya habari Joseph Kusaga, mmiliki wa Clouds Entertainment Group, pamoja na mkewe, Juhayna Kusaga. Longping pia inaungwa mkono na ngazi ya juu ya Wizara ya Kilimo, SAGCOT, na hata Rais wa zamani Kikwete, ambaye amekuwa akitumia nafasi yake kama mkurugenzi wa AGRA kuhamasisha wakulima wa Tanzania kupanda soya kwa ajili ya kuiuzia China.[22] Kama ushahidi wa uhusiano na mtandao wa kisiasa wa Longping, serikali ilimpa kibali maalum kupunguza muda unaohitajika kwa majaribio ya mbegu zake kutoka miaka mitano hadi misimu mitano, hivyo kuwezesha Longping kuanza uzalishaji wa kibiashara mwaka 2024.[23]

Serikali ya Tanzania inafanya pia jitihada ardhi ipatikane kwa kampuni hiyo. Eneo la awali lenye ukubwa wa hekta 53,000 linasemekana limepangiwa kuwa shamba la BBT katika Wilaya ya Chunya, Mkoani wa Mbeya. Longping Tanzania inasema ime "chukua" hekta 10,000 za ardhi hizo kwa ajili ya shamba lake na inadai tayari imeanza kilimo, wakati hekta zilizobaki 43,000 zitapangiwa wakulima washiriki ambao kampuni itawapa mbegu, mbolea, na mashine.[24] Wakulima hao lazima wauze mavuno yao kwa Longping Tanzania pekee, ambayo itayasafirisha kuelekea China, ambapo serikali ya China imeahidi kununua soya yote inayozalishwa.[25]

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Mkurugenzi wa Kampuni ya Yuan Longping High-Tech Agriculture, Liang Shi, nje ya Ikulu. Kulia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde. Februari 17, 2023. [Chanzo: Twitter (X)]

Mipango na matarajio ya Longping ni zaidi ya shamba hili la BBT. Kampuni pia inaanzisha mashamba vitalu na Chama cha Soya Tanzania kilichoundwa hivi karibuni.[26] Kwa mujibu wa mwenyekiti wa chama hicho, Marcus Albany, mashamba vitalu haya yataleta pamoja makundi ya wakulima, na kila mkulima akichangia eneo la ardhi (kiwango cha chini ni hekta 2 na kiwango cha juu ni 10% ya jumla ya shamba kitalu) ili kuanzisha shamba kubwa litakalosimamiwa kama kikundi. Shamba hilo litafanya kazi chini ya mkataba na Longping, ambao unabainisha kiasi ambacho wakulima wanapaswa kuilipa Longping kwa ajili ya kupata pembejeo na mashine pamoja na bei wanayopokea kwa kuuza mavuno yao, na kiasi hicho kinajadiliwa upya kila msimu. Kama ilivyo kwa mashamba ya BBT, mkulima anaweza kuhamisha sehemu yake ya ardhi kwa mkulima mwingine, lakini mkulima huyo lazima achukue shamba hilo kwa masharti sawa yaliyokubaliwa na Longping.

Chama cha Soya Tanzania na Longping tayari wameanzisha shamba kitalu katika Mkoa wa Morogoro, lenye ukubwa wa hekta 5,700 kwa sasa na wanatarajia hatimaye kufikia hekta 10,500. Wako katika mchakato wa kuanzisha shamba kitalu lingine moja mkoani Lindi lenye hekta 10,500, lingine Katavi litakaloanza na hekta 202, na lingine moja Sumbawanga ambalo bado liko katika hatua za majadiliano na mmiliki binafsi wa ardhi. Albany anasema kuwa ingawa chama chake hakijajumuisha vijana, serikali pia inajaribu kuwahusisha katika shamba la BBT mkoani Mbeya.

Wafanyabiashara wengine wa Kitanzania wanaharakisha pia kupata ardhi kwa ajili ya kilimo cha soya. Kampuni ya Jadeja Farming, iliyoanzishwa hivi karibuni, inaanzisha shamba la soya lenye ukubwa wa hekta 2,800 katika ardhi inayogombaniwa na yenye mgogoro katika wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.[27] Kampuni hii ina uhusiano na Kampuni ya Jatu PLC, kampuni iliyoorodheshwa kwenye soko la hisa la kitaifa ambayo ilidai kuwa inashughulika na mashamba vitalu lakini ikaishia kuwatapeli wanahisa wake zaidi ya Dola za Marekani milioni 2.[28] Katika mkoa wa kaskazini wa Kagera, kampuni ya Kitanzania inayoitwa Global Agency inajenga shamba kubwa la hekta 21,000 la mahindi na soya. Licha ya matatizo yake ya zamani ya kisheria na kifedha, Global Agency imepokea kiwango kikubwa cha fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (kupitia mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika), pia kampuni hiyo inaungwa mkono kisiasa na viongozi wa juu wa chama cha Rais Samia.[29]

Zaidi ya hayo, Longping siyo kampuni pekee ya Kichina inayowekeza katika kilimo cha soya nchini Tanzania. Katika mkoa wa pwani wa Kilwa, kampuni inayoitwa Pan Tanzania Agriculture Developments inajishughulisha na mradi mkubwa, wenye ukubwa wa hekta 25,000, wa kilimo cha muhogo na soya, katika ardhi ambayo awali ilikuwa sehemu ya mradi wa jatropha [mibona kaburi] uliokuwa na mgogoro na hatimaye kushindwa vibaya. Pan Tanzania Agriculture Developments ina uhusiano na kampuni ya Kichina, Beijing Chaoliang (inayotambulika kama "Best Agro" au "Super Grain"), pamoja na Hunan Construction Engineering Group na Djibouti Silk Road International Bank.[30] Mwezi Julai 2022, karibu hekta 25,000 zilibadilishwa kutoka kuwa ardhi za kijiji hadi kuwa ardhi za “Ukanda Maalum wa Uchakataji na Usafirishaji” [Export Processing Zone], ikifungua uwezekano wa Pan Tanzania Agriculture Developments kujipatia maeneo hayo kwa mkataba wa muda mrefu.[31]

Migogoro ya ardhi itaongezeka maradufu

Muunganiko wa dhamira mpya ya China kuzalisha na kuagiza soya kutoka Tanzania na kuibuliwa upya kwa mtazamo wa uwekezaji wa kigeni katika kilimo biashara, kwa pamoja inatengeneza mazingira ya kuongezeka kwa uporaji wa ardhi. Migogoro ya ardhi ipo kote nchini, sio kwa sababu tu ya miradi ya kilimo biashara, lakini kwa sababu ya mikataba ya uchimbaji, hifadhi ya misitu na wanyamapori, mbuga za wanyama na miradi ya biashara ya hewa ya ukaa [carbon credit], ambayo serikali inaishadadia. Mojawapo wa hiyo miradi, mradi wa “Misitu Endelevu” ya kampuni inayomilikiwa na mwanachama wa Familia ya Kifalme ya Dubai, inahusisha kutenga hekta milioni nane za ardhi kwa ajili ya kuzalisha mirabaha ya hewa ukaa.[32]

Msukumo mpya wa mashamba vitalu na uzalishaji wa soya unapalilia moto ambao umeshakolea na unawaka. Kwa mfano, katika Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro, mvutano kuhusu ardhi umekuwepo kwa miongo kadhaa kati ya wanakijiji na wakazi ambao wanataka kuendelea kutumia ardhi kwa ajili ya uzalishaji wa chakula na wafanyabiashara ambao wanatumia ardhi hizo ama kwa ajili ya kilimo cha katani, au kwa ajili ya kuyakodisha na kujipatia fedha, au kwa ajili ya kuyahodhi na kueleza kwamba si rafiki kwa ajili ya uzalishaji. Wanakijiji hao hatimaye waliweza kuifanya serikali kuingilia kati, wakati wa urais wa Magufuli na hati miliki zilizokuwa chini ya wafanyabiashara wakubwa zilifutwa. Lakini ardhi hizo hazikurejeshwa kwenye mikono ya wanakijiji; badala yake ilikabidhiwa kwa Halmashauri za Wilaya, ambazo hivi sasa wanayakusanya na kuyakodisha kama mashamba vitalu kwa vinavyoitwa vikundi vya wakulima, ili kuzalisha mazao ya kibiashara kama katani, kwa maelekezo ya serikali au huyakabidhi maeneo hayo kwa wafanyabiashara wakubwa na taasisi za umma, kama Wakala wa Mbegu (ASA).

Abdul Tumbo, mkulima mdogo kutoka kijiji cha Mvumi katika wilaya ya Kilosa, anapambana kuhakikisha ardhi yake haiporwi na wafanyabiashara na skimu za shamba vitalu. [Picha: GRAIN]
Abdul Tumbo ni mkulima kutoka kijiji cha Mvumi katika Wilaya ya Kilosa. Amekamatwa mara kwa mara na kuwekwa gerezani kwa kulima ardhi ambayo wazazi wake walilima lakini ambayo pia inadaiwa kumilikiwa na mfanyabiashara mwenye nguvu. Serikali ya Magufuli ilifuta hati za ardhi za mfanyabiashara huyo miaka michache iliyopita, lakini Halmashauri ya Wilaya [Kilosa] sasa inajaribu kuweka ardhi hiyo katika mfumo wa shamba vitalu, badala ya kuwaruhusu Tumbo na wanavijiji wengine kuendelea na kilimo chao. Wanavijiji na wakazi wa maeneo hayo hawataki kuhusika na mashamba vitalu. Wanasema ardhi ni yao na hakuna sababu ya kulipia kodi. Zaidi ya hayo, wanataka kuzalisha chakula kwa ajili ya familia na jamii zao, si [kuzalisha] bidhaa kwa ajili ya makampuni.[33]

Tumbo anaeleza katika moja ya vijiji jirani Halmashauri ya Wilaya imeendelea na mkakati wake wa mashamba vitalu katika hekta 325 za ardhi ambayo wanakijiji wenyeji wamekuwa wakitumia tangu 1984 ambapo shamba la katani lilipofutwa. Mwezi Desemba 2022, wanakijiji walipanda mahindi ya asili kwa chakula, na muda mfupi baadaye, kwenye ardhi ile ile, "kikundi cha wakulima" kilipanda alizeti. Hivi sasa Halmashauri ya Wilaya imenyang'anya mavuno ya mahindi na uhasama unazidi kuongezeka.
Nchini Tanzania, migogoro kama hiyo inatokea kote huku serikali na wafanyabiashara wakitumia njia za siri kwa njia isiyo halali kuhamisha maeneo makubwa ya ardhi ya vijiji kuwa mashamba ya block kwa ajili ya kuzalisha soya na mazao mengine kwa ajili ya kuuza nje. Maelfu ya wakulima wadogo na wafugaji wanaweza kuondolewa kutoka ardhi zao katika mchakato huu, na wengi zaidi wanaweza kupoteza upatikanaji wa maji, kwani miradi hii mara nyingi inahusisha matumizi ya maji mengi kwa umwagiliaji. Athari zitahisiwa si tu katika maeneo ya vijijini, bali pia katika vituo vya mijini, kwani ardhi ambayo wakulima wadogo sasa wanaitumia kuzalisha chakula kwa nchi itabadilishwa kuwa mashamba makubwa ya kuzalisha mazao kwa ajili ya kuuza nje.

Katika mfano mwingine, mwaka 2023, serikali ilitoa amri, yenye utata, ya kuwafukuza wakazi wa vijiji zaidi ya 23 katika Wilaya ya Mbarali kupitia tangazo la serikali (namba 28 la 2008), amri ambayo utekelezaji wake umesitishwa kwa sababu ya utata na uhalali wa kisheria na kimaadili ya tangazo na amri yenyewe. Amri hii ya kuondoka/ kufukuza inaathiri moja ya wilaya zenye uzalishaji mkubwa na benki ya taifa ya chakula ya mpunga/ mchele na itaathiri zaidi ya wakulima wadogo 25,000 katika eneo hilo. Amri hiyo inakusudia kuongeza na kutanua eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha katika mradi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.[34] Kwa sasa, wakazi 852 wamewasilisha suala hilo Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga amri hiyo ya kuwaondosha na kuwafukuza kwenye maeneo yao.[35]

Hali ya sasa nchini Tanzania inatukumbusha mradi wa ProSavana ambao Japani ilidhamiria kuufadhili miaka kumi iliyopita Kaskazini mwa Msumbiji. Mradi huo ulihusisha kuchukua hekta milioni 14 za ardhi katika moja ya maeneo yenye rutuba na yenye idadi kubwa ya watu nchini kwa ajili ya kuanzisha mashamba makubwa na kuwaingiza na kuwaorodhesha wakulima katika mipango/ utaratibu/ skimu ya kilimo cha mkataba ili kuzalisha soya na mazao mengine ya biashara kwa ajili ya kusafirisha kwenda Japani. ProSavana uliundwa kati ya serikali za Japani, Brazil, na Msumbiji kwa siri, bila ya jamii zitakazoathirika kujua. Punde jamii hizo zilipogundua kilichokuwa kinaendelea, wakaanza kuratibu mapambano, wakishirikiana na asasi za kiraia nchini Msumbiji, Brazili na Japani. Licha ya nguvu kubwa iliyokuwa dhidi yao, wakulima wa Msumbiji na washirika wao walifanikiwa kusitisha mradi huo, na mwaka 2020 mkataba huo ulivunjwa rasmi.[36]

Hiki ni kipindi muhimu kwa wakulima wadogo na wafugaji wa Tanzania kulinda na kutetea ardhi zao. Wazalishaji hawa wa chakula tayari wanakabiliana na ukosefu wa upatikanaji wa ardhi na maji ya kutosha, hali inayochangiwa na mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko kubwa la idadi ya watu nchini. Wanaweza kuzalisha kwa wingi chakula chenye lishe, kisichokuwa na kemikali, kwa ajili ya kuilisha nchi, na hata kuzalisha ziada kwa ajili ya kuuza nje ya nchi, ikiwa sera sahihi na rafiki zitawekwa kusaidia mfumo wa mbegu zao, kuhakikisha ulinzi na usalama katika ardhi na maji yao, na kuhakikisha upatikanaji wa kutosha na wa hakika wa masoko. Rasilimali chache za umma hazipaswi kutumika kwa mipango na modeli ya kilimo kikubwa cha biashara ambacho kimejidhihirisha kutokuwa na mafanikio.


BANGO: Waziri wa Kilimo wa Tanzania, Hussein Bashe, akitembelea mradi wa shamba kitalu katika eneo la Chinangali, Wilaya ya Chamwino, Dodoma. [Chanzo: Twitter (X)]
____________________________________

[1] Oakland Institute, "After Defaulting on Loans, Kilombero Plantation Ltd (KPL) Goes up for Sale," March 2019: https://www.oaklandinstitute.org/after-defaulting-loans-kilombero-plantation-sale
[2] "State tells off Kilombero plantation lobbyists," Daily News, March 2023: https://dailynews.co.tz/state-tells-off-kilombero-plantation-lobbyists/
[3] Kwa baadhi ya mifano, tazama: "Annexe 2. Discarded land deals 2016" in GRAIN, "The global farmland grab in 2016: how big, how bad?", June 2016: https://grain.org/e/5492
[4] SAGCOT pia iliahidi kuanzisha mashamba makubwa kwenye hekta 350,000, kuwahusisha wakulima wadogo 100,000 katika kilimo cha kibiashara, kuunda fursa za ajira mpya 420,000, kuinua watu milioni mbili kutoka kwenye umaskini, na kuzalisha mapato ya kilimo ya dola bilioni 1.2 kila mwaka ifikapo 2030. See: Emmanuel Sulle, "Bureaucrats, investors and smallholders: contesting land rights and agro-commercialisation in the Southern agricultural growth corridor of Tanzania", Journal of Eastern African Studies, 2020, DOI: 10.1080/17531055.2020.1743093
[5] Gideon Tups and Peter Dannenberg, "Emptying the Future, Claiming Space: The Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania as a Spatial Imaginary for Strategic Coupling Processes", Geoforum 123, 2021: https://doi.org/10.1016/j.geoforum.2021.04.015
[6] “Tanzania government cancels Sh100bn Sagcot scheme,” The Citizen, May 2023: https://www.thecitizen.co.tz/tanzania/news/national/tanzania-government-cancels-sh100bn-sagcot-scheme-2681476
[7] "Magufuli Revokes Title Deeds for 14 Undeveloped Farms," Tanzania Daily News, August 2017: https://allafrica.com/stories/201708150094.html
[8] Mazungumzo binafsi na Prudence Lugengo, Mtaalam wa Sera wa SAGCOT, 24 March 2023.
[9] Serikali iliongeza bajeti ya rasilimali za umwagiliaji kutoka 57bn/- mwaka 2021-22 hadi 416bn/- mwaka 2022-23 na ina lengo la kufanya upanuzi wa eneo la umwagiliaji kutoka hekta 727,280 hadi hekta 822,285 ifikapo mwaka 2022/2023, na lengo la kitaifa la umwagiliaji ni hekta 1.2 milioni kufikia mwaka 2025 na hekta 8.5 milioni ifikapo mwaka 2030.
[10] Wazo la mradi linaelezwa kutoka kwa Geoffrey Kirenga, Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT
[11] "Tanzanian government to draft 52,000 JKT members into BBT scheme," The Citizen, July 2023: https://www.thecitizen.co.tz/tanzania/news/national/tanzanian-government-to-draft-52-000-jkt-members-into-bbt-scheme-4299870
[12] Taarifa kuhusu mashamba vitalu zimekusanywa kutoka kwenye ripoti mbalimbali za habari, nyaraka za serikali, na mahojiano na watu mbalimbali waliohusika katika programu hiyo mwezi Machi na Aprili 2023.
[13] "BBT bring hope for youth employability," The Guardian, March 2023: https://www.ippmedia.com/en/features/bbt-brings-hope-youth-employability
[14] Mwezi Julai 2022, Dewji alikiambia chombo cha habari cha Reuters kwamba ana mpango wa kuorodhesha kampuni ya kilimo yenye thamani ya hadi Dola bilioni 4 kwenye masoko ya hisa ya New York au London ifikapo 2023, kwa fedha zilizopatikana hasa kutoka benki za maendeleo. Rachel Savage, "Tanzanian entrepreneur Dewji plans $2-4 billion grains production investment via SPAC," Reuters, July 2022: https://www.reuters.com/markets/deals/tanzanian-entrepreneur-dewji-plans-2-4-bln-grains-production-investment-via-spac-2022-07-08/
[15] "Tanzania revokes titles to six farms owned by Dewji," East African, January 2019: https://www.theeastafrican.co.ke/tea/news/east-africa/tanzania-revokes-titles-to-six-farms-owned-by-dewji--1410744
[16] Tazama uzi wa Maria Sarungi Tsehai (@MariaSTsehai), 27 January 2024 katika Twitter (X): https://twitter.com/MariaSTsehai/status/1751133786195087548?t=Rbeb-qm73R83MVzH6UFt-g&s=19
[17] Tazama hotuba ya bajeti ya 2023 ya Mheshimiwa Dr. Situmbeko Musokotwane, Waziri wa Fedha: https://www.parliament.gov.zm/sites/default/files/documents/articles/2023%20Budget%20Speech.pdf; na Tamko la Kiwizara la Waziri wa Kilimo, lililowasilishwa bungeni Machi 16, 2023 na Mh. Mtolo Phiri, MP, kuhusiana na Programu ya Maendeleo ya Shamba Kitalu: https://www.parliament.gov.zm/sites/default/files/images/publication_docs/Ministerial%20Statement%20-%20On%20the%20Farm%20Block%20Development%20Programme.pdf
[18] Owen Khamula, "Agriculture ministry moves in to establish mega farms," Nyasa Times, 30 June 2022: https://www.farmlandgrab.org/31400
[19] "Tanzania Country Presentation for HIH Investment Forum," October 2023: https://www.fao.org/docs/handinhandlibraries/countries/tanzania/bbt_ps_m-m_presentation-raf-slide-wg-25-sept.pdf?sfvrsn=1dad93cf_1 and "USAID to invest $100M in supporting agribusiness youth in Tanzania," Further Africa, November 2023: https://furtherafrica.com/2023/11/17/usaid-to-invest-100m-in-supporting-agribusiness-youth-in-tanzania/
[20] "First Shipment of Tanzanian Soybeans Enter China" June 2021: http://en.sasac.gov.cn/2021/06/25/c_7280.htm
[22] "Good news for soybeans farmers to effectively utilise Chinese market," The Citizen, February 2022: https://www.thecitizen.co.tz/tanzania/news/business/good-news-for-soybeans-farmers-to-effectively-utilise-chinese-market-3721346
[23] Mawasiliano binafsi na Juhayna Kusaga, Mkurugenzi wa Longpin Tanzania, Machi 21, 2023
[24] Mawasiliano binafsi na Juhayna Kusaga, Mkurugenzi wa Longpin Tanzania, Machi 21, 2023 na Novemba 27, 2023
[25] "Wakulima wa kusini wavutiwa na uwekezaji wa kampuni ya Longping High Tech", Ministry of Foreign Affairs and East African Cooperation (Tanzania), May 2022: https://www.foreign.go.tz/resources/view/wakulima-wa-kusini-wavutiwa-na-uwekezaji-wa-kampuni-ya-longping-high-tech
[26] Mawasiliano binafsi na Marcus Albany, Machi 24, 2023
[27] Tazama tovuti ya kampuni: http://jadeja.co.tz/about/. Na video kuhusu shamba: https://www.youtube.com/watch?v=oZJf5eA0X64&ab_channel=JadejaFarming. Shamba linafahamika kama Shamba la Efatha, ambalo liliingia kwenye mgogoro wa ardhi, tazama: ‘We were wrong on farm dispute’, The Citizen, October 2017: https://www.thecitizen.co.tz/tanzania/news/national/-we-were-wrong-on-farm-dispute--2609534
[28] Mkurugenzi wa Jadeja, Hussein Msemwa alikuwa Meneja Msaidizi wa JATU PLC (https://www.linkedin.com/in/hussein-msemwa-07246211b/?originalSubdomain=tz). Kwa taarifa zaidi kuhusu JATU PLC, tazama: "Struggling Jatu Plc turns to Dutch consultant", The Citizen, January 2023: https://www.thecitizen.co.tz/tanzania/news/business/struggling-jatu-plc-turns-to-dutch-consultant--4075174
[29] Kuhusiana na changamoto za kisheria na kifedha, tazama kesi dhidi ya Global Agency kwa kushindwa kuilipa Rabobank (https://tanzlii.org/tz/judgment/high-court-commercial-division/2020/51; https://tanzlii.org/tz/judgment/high-court-commercial-division/2021/3517) na Balton Tanzania (https://tanzlii.org/tz/judgment/high-court-commercial-division/2022/378). Kuhusiana na kuungwa mkono na Chama cha Mapinduzi (CCM) Makamu Mwenyekiti Colonel Abdulrahman Kinana, tazama: https://panafricanvisions.com/2022/09/tanzania-ruling-party-vice-chairperson-welcomes-investors-in-kagera-region-which-is-suitable-for-opportunities/; na kutoka kwa Waziri wa sasa wa Kilimo, Hussein Bashe, tazama: https://www.ippmedia.com/en/news/bashe-orders-misenyi-dc-support-investors-promote-agro-investments. TADB haitoi taarifa hadharani kuhusu ufadhili wake kwa makampuni, hata hivyo, ripoti ya AfDB kuhusu mkopo wake kwa TADB inaonyesha kuwa Global Agency ilipokea fedha kutoka TADB kwa ajili ya shamba la Kagera na kwamba 45% ya jumla ya mkopo wa AfDB wa Dola milioni 67 ulikwenda kwa makampuni mkoani Kagera (ambapo kampuni nyingine iliyoorodheshwa ni Kagera Cooperative Union). Tazama: https://www.afdb.org/en/documents/tanzania-tanzania-agricultural-development-bank-project-completion-report
[30] "Chaoliang Group's Tanzania PTA construction project signed with Hunan Construction Engineering Group for USD 300 million," China Agricultural Outlook News, October 2021: https://www.farmlandgrab.org//31442. Hunan Construction Engineering Group ilichukuliwa hatua mwaka 2013 na World Bank kwa vitendo vya udanganyifu katika mradi wa ujenzi wa barabara nchini Tanzania: https://www.worldbank.org/content/dam/documents/sanctions/office-of-suspension-and-debarment/2018/nov-1/Notice-of-Uncontested-Sanctions-Proceedings-Case-268.pdf
[32] "Blue Carbon and the Government of Tanzania join forces to accelerate transition to low-carbon economy," Gulf news, February 2023: https://gulfnews.com/business/corporate-news/blue-carbon-and-the-government-of-tanzania-join-forces-to-accelerate-transition-to-low-carbon-economy-1.1675752836855
[33] Mahojiano na Abdul Tumbo, Machi 29, 2023
[34] “World Bank investigating alleged crimes at $150 million Ruaha tourism project,” The Citizen, September 2023 https://www.thecitizen.co.tz/tanzania/news/national/world-bank-investigating-alleged-crimes-at-150-million-ruaha-tourism-project-4384506
[35] “Smallholders In Mbarali Protest Govt Plans To Evict Them From Their Land,” The Chanzo, February 2023: https://thechanzo.com/2023/02/09/smallholders-in-mbarali-protest-govt-plans-to-evict-them-from-their-land/
[36] Kwa taarifa zaidi kuhusiana na ProSavana tazama: https://www.farmlandgrab.org/cat/show/827
Author: GRAIN and La Via Campesina Southern and Eastern Africa
Links in this article:
 • [1] https://grain.org/admin/articles/6662/edit#sdfootnote33sym
 • [2] https://www.oaklandinstitute.org/after-defaulting-loans-kilombero-plantation-sale
 • [3] https://dailynews.co.tz/state-tells-off-kilombero-plantation-lobbyists/
 • [4] https://grain.org/e/5492
 • [5] https://doi.org/10.1016/j.geoforum.2021.04.015
 • [6] https://www.thecitizen.co.tz/tanzania/news/national/tanzania-government-cancels-sh100bn-sagcot-scheme-2681476
 • [7] https://allafrica.com/stories/201708150094.html
 • [8] https://www.thecitizen.co.tz/tanzania/news/national/tanzanian-government-to-draft-52-000-jkt-members-into-bbt-scheme-4299870
 • [9] https://www.ippmedia.com/en/features/bbt-brings-hope-youth-employability
 • [10] https://www.reuters.com/markets/deals/tanzanian-entrepreneur-dewji-plans-2-4-bln-grains-production-investment-via-spac-2022-07-08/
 • [11] https://www.theeastafrican.co.ke/tea/news/east-africa/tanzania-revokes-titles-to-six-farms-owned-by-dewji--1410744
 • [12] https://twitter.com/MariaSTsehai/status/1751133786195087548?t=Rbeb-qm73R83MVzH6UFt-g&s=19
 • [13] https://twitter.com/MariaSTsehai/status/1751133786195087548?t=Rbeb-qm73R83MVzH6UFt-g&s=19
 • [14] https://www.parliament.gov.zm/sites/default/files/documents/articles/2023%20Budget%20Speech.pdf
 • [15] https://www.parliament.gov.zm/sites/default/files/images/publication_docs/Ministerial%20Statement%20-%20On%20the%20Farm%20Block%20Development%20Programme.pdf
 • [16] https://www.farmlandgrab.org/31400
 • [17] https://www.fao.org/docs/handinhandlibraries/countries/tanzania/bbt_ps_m-m_presentation-raf-slide-wg-25-sept.pdf?sfvrsn=1dad93cf_1
 • [18] https://furtherafrica.com/2023/11/17/usaid-to-invest-100m-in-supporting-agribusiness-youth-in-tanzania/
 • [19] http://en.sasac.gov.cn/2021/06/25/c_7280.htm
 • [20] https://www.clbrief.com/longping-high-tech-to-quintuple-seed-production-capacity-in-brazil/#:~:text=LongPing
 • [21] https://www.clbrief.com/longping-high-tech-to-quintuple-seed-production-capacity-in-brazil/#:~:text=LongPing%20is%20developing%20these%20soybean,considered%20small%20by%20the%20Chinese
 • [22] https://www.thecitizen.co.tz/tanzania/news/business/good-news-for-soybeans-farmers-to-effectively-utilise-chinese-market-3721346
 • [23] https://www.foreign.go.tz/resources/view/wakulima-wa-kusini-wavutiwa-na-uwekezaji-wa-kampuni-ya-longping-high-tech
 • [24] http://jadeja.co.tz/about/
 • [25] https://www.youtube.com/watch?v=oZJf5eA0X64&ab_channel=JadejaFarming
 • [26] https://www.youtube.com/watch?v=oZJf5eA0X64&ab_channel=JadejaFarming
 • [27] https://www.thecitizen.co.tz/tanzania/news/national/-we-were-wrong-on-farm-dispute--2609534
 • [28] https://www.linkedin.com/in/hussein-msemwa-07246211b/?originalSubdomain=tz
 • [29] https://www.thecitizen.co.tz/tanzania/news/business/struggling-jatu-plc-turns-to-dutch-consultant--4075174
 • [30] https://tanzlii.org/tz/judgment/high-court-commercial-division/2020/51
 • [31] https://tanzlii.org/tz/judgment/high-court-commercial-division/2021/3517
 • [32] https://tanzlii.org/tz/judgment/high-court-commercial-division/2022/378
 • [33] https://panafricanvisions.com/2022/09/tanzania-ruling-party-vice-chairperson-welcomes-investors-in-kagera-region-which-is-suitable-for-opportunities/
 • [34] https://www.ippmedia.com/en/news/bashe-orders-misenyi-dc-support-investors-promote-agro-investments
 • [35] https://www.afdb.org/en/documents/tanzania-tanzania-agricultural-development-bank-project-completion-report
 • [36] https://www.farmlandgrab.org/31442
 • [37] https://www.farmlandgrab.org//31442
 • [38] https://www.worldbank.org/content/dam/documents/sanctions/office-of-suspension-and-debarment/2018/nov-1/Notice-of-Uncontested-Sanctions-Proceedings-Case-268.pdf
 • [39] https://www.utumishi.go.tz/uploads/documents/sw-1665955257-23%20SEPTEMBA,%202022.pdf
 • [40] https://www.utumishi.go.tz/uploads/documents/sw-1665955257-23%20SEPTEMBA,%20%202022.pdf
 • [41] https://gulfnews.com/business/corporate-news/blue-carbon-and-the-government-of-tanzania-join-forces-to-accelerate-transition-to-low-carbon-economy-1.1675752836855
 • [42] https://www.thecitizen.co.tz/tanzania/news/national/world-bank-investigating-alleged-crimes-at-150-million-ruaha-tourism-project-4384506
 • [43] https://thechanzo.com/2023/02/09/smallholders-in-mbarali-protest-govt-plans-to-evict-them-from-their-land/
 • [44] https://www.farmlandgrab.org/cat/show/827