https://grain.org/e/5780

Nguo Mpya za Ukoloni: Mikataba ya Ushirikiano wa Kiuchumi (EPAs) kati ya Umoja wa Ulaya (EU) na Afrika

by GRAIN and Kenya Food Rights Alliance (KeFRA) | 21 Aug 2017

 

Jumuiya ya Jamii ya 2007: Wajumbe wanaadhamana Nairobi dhidi ya EPAs. SwissInfo

Tangu mwaka wa elfu mbili na mbili (2002), mataifa ya Afrika, Caribbean na Pacific (ACP), yamehusika kwa mazungumzo ya makubaliano ya kibiashara yenye usawa, yajulikanayo kama, Mkataba wa Muungano wa Kiuchumi (EPA) na Umoja wa Ulaya (EU). Na kwa vile iliangaziwa kuwa ushindi mkuu kwa mataifa ya ACP katika nyanja ya kujiendeleza kiuchumi na katika ukuzaji wa viwanda, ukweli ni kwamba ni makubaliano yenye mfumo wa kikoloni yanayofaidi upande mmoja.

Hata ingawa haijapata kutangazwa sana, EPA imeendelea kupata upinzani kutoka kwa mataifa ya ACP, juu ya madhara yake kwa wakulima wadogo. Baadhi ya mataifa ya Afrika ambayo yameangaziwa hapa yaonyesha jinsi jamii zinapigania kuchukua tena mamlaka dhidi ya mali yao na kulinda soko zao kutokana na wingi wa bidhaa duni, dawa za kupulizia mimea, pamoja na bidhaa zenye viini vinasaba (GMOs), ambazo zimeingia sokoni mwao kutoka mataifa ya EU. 

"... tani moja ya kakao ni takribani dola 1300 ya kimarekani, wakati gari moja ya 4 * 4 ni tarkriban dola 120,000 za kimarekani. Hivyo basi unahitaji takribani tani 92 za kakao ili kubadilishana na gari moja ya 4 * 4. Lakini ili kupata tani moja, unahitaji ekari za shamba zisizopungua 20. Mkulima wa wastani wa kakao nchini Ghana anamiliki kama ekari 2-3 pekee, kumaanisha itachukua miaka zaidi ya 500 kuzalisha kakao ya kutosha kununua gari ya 4 * 4." 
John Opoku, mwanasheria wa haki za kibinadamu na mwanaharakati kutoka Ghana.

Kauli hii inaonyesha suala la kutisha la kibiashara ambalo Waafrika na watu wengine wa mataifa ya kusini, wanakumbana nalo kila siku. Tangu enzi, mataifa ya kusini yameingia katika mikataba ya biashara na mataifa ya dunia isiyowafaidi. Aina ya biashara inayofuata mikataba hii inafaidi upande mmoja pekee – na kuweka haya mataifa katika hali ya umaskini daima! Ya maslahi maalum, ni FTAs zinazochipuka mara kwa mara, mojawapo ikiwa ni EPA.

Tangu mwezi wa tisa, 2002, mataifa ya ACP yamekuwa yakijadiliana EPA ili kuwe na usawa katika mipango ya biashara na EU, chini ya Mkataba wa Cotonou. Hii Mikataba ya EPAs ina lengo la kueneza soko huru kwenye uchumi wa mataifa yaliyokuwa chini ya ukoloni wa Ulaya, hatua ambayo itakuwa na madhara makubwa kwa wakulima, wavuvi, wachimbaji, wafanyakazi na watumiaji kote katika kanda zinazohusika.

Kabla ya EPAs, nchi za ACP zilikua na mipango pendelezi ya biashara na EU.  Mojawapo ni biashara ya ‘Kila Kitu Ila Silaha’ (Everything But Arms - EBA), mpango ambao unaegemea upande mmoja ili kufungulia nchi zisizoendelea, masoko ya EU, na hivyo kutotoza nchi hizo ushuru na kuwapa soko huru kule EU. Ingawa nafasi ilikuwepo, nchi za ACP zilifaulu mara chache tu kutimiza kiwango walichotarajiwa kuuza nchi za EU chini ya EBA. Kwa mfano, Uganda ina nafasi kuuza tani 5000 za sukari huko EU, lakini mauzo yao ya nje katika EU kamwe hayakufika kiasi hiki, sababu ikiwa ni masharti magumu ya EU sharia ya chanzo, na vikwazo vya uwezo wa utoaji.

Nguzo iliyotumiwa na EU kubadili kutoka EBA na kuanzisha EPA na mataifa ya ACP, ilikuwa hoja kuwa biashara ya upendeleo haikuwa ikifuata mapendekezo ya Shirika la Biashara Duniani (WTO). Huu ulikuwa ni ujanja kwani vizuizi katika sheria ya WTO vinaweza kuondolewa. Wazo lao kweli lilikuwa ni kushinikiza soko huru zaidi katika kikanda cha ACP ili kufaidi fedha za Ulaya (wauzaji wa nje kwanza, wawekezaji baadaye), ili kujenga soko la kimataifa lililo na sheria sawa kila mahali. Ilidhaniwa kwamba nchi za ACP zingefaidika na zingejikuza zaidi kupitia uongezefu wa kazi na uhamishaji wa teknolojia. [1]

Kwa kweli, ahadi katika EPA sio tofauti na zile ambazo tulizoziona na kuzisikia wakati wa ahadi za mambo makubwa ambazo zilipewa makazi katika Mipango ya Marekebisho ya Miundo (Structural Adjustment Programmes - SAPs) ambayo hayakufaulu kamwe - athari ambazo bado zinashuhudiwa hata waleo!   Zote zina mizizi ndani ya mfumo wa kikoloni ambao unaruhusu EU na makampuni mengine ya huko Kaskazini, kudondoa malighafi kutoka mataifa haya wakitumia masharti yao wenyewe.  Kama vile inavyofanyika kwa FTAs, EPAs pia zinahitaji kuchambuliwa na kueleweka kama mfululizo wa mambo yanayoingiliana, na yanayojadiliwa moja baada ya nyingine, yakilenga kupooza ukuzaji wa nchi zinazojitokeza kiuchumi.

Badala ya kutafuta FTAs ​​baina ya nchi kwa nchi na mataifa yote 79 ya ACP, Ulaya iligawanya mataifa ya ACP kwenye kambi 7- Afrika Magharibi, Afrika kati, Afrika Mashariki na Kusini (ESA), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Afrika Kusini (SADC), Caribbean na Pacific.  Mchakato huo uliangazwa kama njia inayoimarisha ushirikiano wa kikanda.  Lakini tangu kuanzishwa mwezi wa tisa 2002, kumekuwa na migawanyiko na chuki, muda wa kumaliza makubaliano haujatimizwa na vile mambo yalivyo sasa, yamechanganyika sana, hasa katika bara la Afrika. 

Hali Ilivyo ya EPA

 Picha hii inaonyesha makundi ya kikanda katika hatua mbalimbali za kutia sahihi au kujadili EPA. Hivi sasa, Caribbean tu ndio imeingia kwenye EPA vikamilifu ilhali makubaliano ya Afrika na Pasifiki yamerudishwa nyuma na kuwa maandishi ya muda mfupi ambayo yanahusu biashara ya bidhaa tu kwa sasa. Huko Afrika Magharibi, kwa mfano, nchi zote zimetia sahihi isipokuwa Nigeria, Gambia na Mauritania. Katika Afrika ya Kati, Cameroon pekee ilivunja safu na kuweka sahihi. Ikumbukwe kwamba chini ya shinikizo la Brussels, nchi zote hizi zilijadiliana kama vitengo vya kikanda chini ya matarajio ya kwamba wataweka sahihi kama kitengo. Hii inamaanisha kwamba Kenya, kwa mfano, haitafaidika na EPA mpaka nchi zote za EAC zidhibitishe na zikubaliane na mpango huo. Kinyume cha matarajio, ni dhahiri kwamba mbinu hii haikufanya mengi kwa mchakato wa ushirikiano wa kikanda cha Afrika.

Vile EPAs inavyoathiri chakula na wakulima 

Tangu mwanzo, EPA imekuwa na utata. Hii inatokana na vifungu vingine vilivyojumuishwa katika makubaliano ambayo yanasababisha vitisho vikali kwa haki za binadamu na ubinafsishaji wa sekta muhimu katika uchumi wa nchi. Hii ni kweli hasa katika nchi nyingi za Afrika. Pamoja na kudhoofisha uhuru wa kitaifa, EPAs imepunguza taratibu za ushirikiano wa kikanda, imeweka vaikwazo vya viwanda vya mitaa, na wamezuia mashirika ya kiraia kuchangia sera. Ya maslahi maalum ni madhara ya EPA kwa kilimo cha Afrika, hasa kilimo cha wakulima wadogo, ambacho ni uti wa mgongo wa uchumi wa mataifa mengi ya Afrika. [2]

Asilimia tisini ya wakulima wote Afrika ni wakulima wadogo ambao wanatumia asilimia kumi na tano tu ya ardhi ya kilimo barani Afrika; pia, wanachangia asilimia tisini ya mbegu inayotumika Afrika. Wakulima wadogo huchangia asilimia dhemanini ya chakula katika maeneo haya.  Wanawake nao wanajumuisha karibu asilimia arobaini na tatu ya wanaofanya kazi ya mashambani, Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara. 

Pia, inakadiriwa kuwa sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki inaajiri karibu watu milioni kumi na tatu Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Uchugaji huwapa mapato watu milioni hamsini, milioni 12-22 wakiwa katika Pembe ya Afrika. Pamoja na haya kuna sekta ya mashamba makubwa ambayo hulenga kuuza bidhaa kama vile ndizi, miwa, kakao, mananasi, chai na kahawa, nje mwa bara. [3]

Wakulima wadogo wa Afrika huzalisha ili kulisha jamii zao na kuuza sokoni, na hawana uwezo wala nia ya kuuzia soko la Ulaya. Takwimu zinaonyesha kuwa wingi wa bidhaa za viwanda vya EAC huuzwa kwa Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) ilhali malighafi huuziwa soko la EU.

Kuweka huru soko la EAC ina maana kwamba bidhaa duni na bidhaa zenye ruzuku kutoka EU zitaingia kwa urahisi katika kikanda, na hatimaye kudhoofisha sekta ya viwanda. Kwa hivyo, wana mengi ya kupoteza kutoka kwa makubaliano ya FTA na Ulaya, kwani makubaliano hayo yatawezesha vyakula vya Ulaya kujaza soko za Afrika na kuhamisha vile vya wenyeji, na pia itafungulia mlango makampuni ya Ulaya kuanzisha mashamba mengi makubwa ya madola, mashamba ya ufugaji samaki na shughuli zingine za mauzo ya bidhaa za kilimo. Haya yote yataadhiri upatikanaji wa ardhi, maji, mbegu na masoko. [4]

Uzoefu tayari waonyesha ya kwamba, EPAs haziwanufaishi Waafrika ila zimo ili kufungulia makampuni ya Ulaya yaingie Afrika na yazalishe bidhaa na mali kwa ajili ya soko lao wenyewe.

Ukiangazia kesi ya Afrika Mashariki utaratibu huu tayari unadhoofisha ustawi wa chakula cha watu wengi na kuharibu mazingira. Ziwa Viktoria, ambalo ni la maji safi ni la pili kwa ukubwa duniani lipo Afrika Mashariki. Ziwa hili lina aina nyingi ya samaki ambazo hupatia wengi mapato na ulishaji katika kanda hii.

Hata hivyo, wenyeji wa Afrika Mashariki hawana uwezo wa kununua samaki hao, ila wanaweza tu kununua “mgongo wazi” (mifupa ya samaki). Mgongo wazi ni mabaki kutoka kwa makampuni ya samaki ambayo hufanya usindikaji wa Mbuta (Nile Perch) ya kuuza Ulaya. Hii, pamoja na uzalishaji wa maua, kakao, pamba, maharagwe, na kahawa, inahakikisha kuwa mazao ya Kiafrika yananufaisha soko la EU. 

Manufaa ya EPA Kwa soko la EAC 

Nia ya majadiliano ya EPA ni kufungua masoko ya mataifa ya Afrika na pia kurahisishia makampuni ya Ulaya yaingie masoko ya Afrika. Kwa hiyo, nchi za Kiafrika, kama nchi nyingi za ACP, zililazimishwa kufungulia bidhaa za Ulaya, masoko yao kama ilivyoonyeshwa kwa ratiba ifuatavyo.

Bila kuangalia kwa undani, ratiba hii inatumika kulinda viwanda changa na bidhaa nyeti. Uchunguzi wa makini, hata hivyo, unaonyesha wazi wazi upungufu uliopo katika ratiba.

Kwa mfano, kwa upande mmoja, EAC imehifadhi unga wa mahindi (Kanuni ya HS, tarakimu 6 110220) kwa kiwango cha ushuru cha 50%. Kwa upande mwingine, wanga wa mahindi (Kanuni ya HS, nambari 6 110812), itokayo kwa unga wa mahindi, haitoshwi ushuru. Haya mambo kana yanadhuru bidhaa nyingine, kama viazi. Katika ratiba hii, soko huru, kuongeza thamani kwa njia ya usindikaji wa bidhaa za kilimo utazuiliwa, na pia itaathiri uhakika wa chakula kwa sababu ya uhusiano wa kina kati ya kilimo na viwanda.

Baadhi ya mataifa ya EU pia imo katika Ushirikiano Mpya wa G7 wa uhakika wa Chakula na Lishe (NAFSN), ambao unashughulikia moja kwa moja upanuzi katika Afrika wa makampuni makubwa ya kilimo na makampuni ya chakula kama Bayer na Unilever. Kwa ugani, mataifa haya yamehusishwa kwa mpango wa kupanua masoko ya EU huku Afrika, ili EU wauze dawa za wadudu, mbegu za viini vinasaba, na vyakula duni.

Zaidi ya hayo, makampuni ya mbegu yanakabiliana na masoko yaliyofurika mbegu kama vile, Marekani Kaskazini, Ulaya na Japan. Kwa hivyo wanaendelea kushinikiza Afrika kufungua masoko yake kwa bidhaa zao. Kwa mfano, mwenyekiti wa Syngenta Ren Jianxin anatamani kuikuza maradufu kampuni ya Syngenta katika kipindi cha miaka mitano hadi kumi ijayo. Jianxin tayari ameonyesha kwamba upanuzi wake utafanyika hasa nchini India na katika mataifa ya Afrika. [5]

Haya yanasababisha nchi za Afrika ziwe kwenye hatari ya kununua bidhaa nyingi zisizohitajika, hizi zikiwa ni pamoja na, kupenya kwa GMOs. Mara tu mazao haya ya vinasaba yatakapofanikiwa kuingia katika nchi kadhaa, itakuwa vigumu kwa nchi zingine za Afrika kupinga.

Katika nchi nyingi, GMOs huangaziwa kama jibu la maswala ya ustawi wa uhakika wa chakula. Anne Maina kutoka shirika la Kenya Biodiversity Coalition (KBioC) ana wasiwasi juu ya kuingizwa kwa GMO nchini Kenya. [6]

Licha ya marufuku zilizopo kwenye uagizaji wa GMOs katika Kenya, nchi imekuwa na udhibiti mdogo juu ya kuingia kwa vyakula vya GMO, hasa katika nyakati za uhaba wa chakula. Kwa sababu hii, mwaka 2017, National Biosafety Authority Kenya (NBA) ilionya hadharani wafanyabiashara juu ya uagizaji wa bidhaa za nafaka kama nafaka, baadhi ya bidhaa za cornflakes na bisi. Kenya ina uchumi wenye nguvu katika Afrika Mashariki na inaweza kuweka historia kwa nchi nyingine katika bara la Afrika, hasa Nigeria na Ghana ambazo zimechukua hatua za kuboresha utoaji kitaifa kwa teknolojia ya mimea na usalama wa viumbe. [7]

Jumuiya ya Africa Mashariki (EAC) wa kufikia soko kutoa chini ya EPA 

Picha hii inaonyesha pendekezo la kuingia soko la EAC. Pendekezo hili linalazimisha mataifa ya EAC, kupitia hatua tatu, kufungulia bidhaa kutoka EU, soko yao kwa kipindi cha miaka 25. [8]

Katika makubaliano ya EPA, mataifa husika yanatarajiwa kukata ushuru wa hali ya juu sana. EAC kwa mfano, imejitolea kulegeza soko la uagizaji kwa asilimia 80 katika kipindi cha miaka zaidi ya kumi na tano; hii hatua itaadhiri malighafi na bidhaa muhimu ambazo tayari hazitoshwi ushuru. Hatua kama hiyo inaingiza sekta ya kilimo katika ushindani usio wa haki na EU, ambayo bila shaka itatikisa msingi wa biashara za kikanda, na kuwaondoa sokoni wakulima asili sababu ya ushindani wa bidhaa duni kutoka EU. Kwa hivyo, bidhaa “nyeti” zitatengwa ili zisitozwe ushuru na kubaki zikiwa zimepewa “ulinzi” kwa sasa.

Maziwa ni mojawapo ya bidhaa nyeti humu Afrika na hii imesababishwa na kuwa tunauziwa na wakulima wadogo wa mifugo ambao hawawezi shindana na bidhaa za kilimo zenye ruzuku kutoka Ulaya. Cha kutia moyo ni kwamba, kanda zingine zimechagua kulinda sekta zao za maziwa. Katika Afrika Mashariki, bidhaa zote za maziwa zitakuwa zimetengwa zisipate madhara kama EPA itasahihiswa. Kwa mfano, serikali ya Kenya ilipogundua kwamba maisha ya wakulima wa maziwa karibu 600,000 itaadhirika vibaya kutokana na uagizaji wa maziwa ya unga na maziwa kutoka EU, iliamua kuorodhesha maziwa kama mojawapo wa bidhaa nyeti humu nchini. Katika Afrika Magharibi, uagizaji wa bidhaa za maziwa isipokuwa maziwa ya unga, umepigwa marufuku ambapo Nigeria ndio nchi kuu inayoagiza maziwa humo. Kwa upande wa Afrika ya Kusini, baadhi ya nyama na maziwa zimetengwa, lakini si zote. [9]

Uvuvi ni sekta nyingine inayotishiwa na EPA katika nchi za Afrika. Ushuru wa biashara ya bidhaa za samaki umeundwa kwa wazi ili kulinda soko la bidhaa za samaki la EU, na kuwapa uwezo wa kununua bidhaa za samaki kwa bei ya chini kabisa katika masoko ya Afrika. Kwa sababu ya tofauti kubwa kati ya ushuru wa samaki unaotozwa ili kuingizwa masoko ya EU, uvuvi wa Kiafrika unalazimika kuuza samaki bila kupata faida, ilhali bidhaa za samaki za EU zaendelea kujaza masoko ya Afrika.

Kuwekwa huru kwa sekta ya uvuvi hakujafaidi wavuvi wadogo wadogo, lakini kinachoshuhudiwa ni kuongezeka kwa visa vya: wenyeji wasio na uwezo wa kununua samaki, uvuvi wa samaki kinyume cha sheria karibu na maeneo ya pwani, na kupungua kwa samaki sababu ya uvuvi zaidi kupindukia. [10]

Sekta ya Maua na Makampuni ya Mbegu huhamasisha Mikataba ya biashara kati ya Kenya na EU

Kenya hivi karibuni imetia sahihi na kuthibitisha vyombo vyake kuwa sehemu ya makubaliano ya ushirikiano wa uchumi (EPAs) wa EU na EAC. Shinikizo la kwanza la kusahihiisha ilikuja kutoka kwa sekta ya kuuza nje ya maua yenye thamani kubwa inayoendeshwa na wakulima matajiri wachache wa kigeni na makampuni ya Kimataifa.

Faida ya mauzo ya maua haifikii raia wa kawaida kwa kuwa makampuni haya ya kimataifa yanashiriki katika miradi tata ya kuepuka kodi. Mwaka 2011, Christian Aid iliripoti kuwa Kenya inaweza kuwa inapoteza dola milioni mia tano kila mwaka, kama „kutoroshwa kwa fedha“ kutokana na biashara yake ya maua na EU. [11]

Kwa upande mwingine, sekta ya maua ilikuwa mstari wa mbele kusukuma Kenya kutia sahihi Mikataba ya Ulinzi wa Aina Mpya za Mimea (UPOV) ya mwaka 1991.

Kenya kukimbilia kuwa wa kwanza kuingia mikataba ya EPA na UPOV 1991, inaleta wingu la giza kwa wakulima wadogo na kuhatarisha haki ya chakula. Ni mbaya kwa Kenya kutarajia nchi nyingine za wanachama wa EAC kutia sahihi na kuthibitisha EPA hii. Kwa kukimbilia kukutia sahihi Sheria ya Upatikanaji wa Soko na EU, serikali ya Kenya ilizunguka hukumu ya mahakama ya Kenya kuwa kuna mashauriano ya kutosha na wakulima wadogo wa Kenya na kwamba wanahusika katika mazungumzo kama wadau muhimu. Kama ilivyo kwenye EPA, sehemu kubwa ya mzigo kwa Kenya kujiunga na UPOV iliyofanya kuwavuta wengine wa nchi za EAC pamoja, ilitokana na ukulima wa maua na viwanda vya mbegu, ambavyo vilitaka kuhakikisha kanda hii imefumwa na biashara kwa manufaa yao wenyewe. [12] 

Daniel Maingi, Mratibu wa Taifa wa Kenya Food Alliance (KeFRA) na pia Mkurugenzi wa Growth Partners Africa.

Makubaliano ya kujadili baina ya sekta ya mbegu

Kama ilivyotajwa, EPAs baina ya EU na Afrika zinahusu tu biashara ya bidhaa kwa sasa. Lakini zina kifungu ambacho kinasema kuwa katika kipindi cha miaka mitano, wajumbe watajadili zaidi chini ya kipengele zaidi chini ya Kifungu cha Marudiano (Rendezvous Clause). Kifungu hiki kinasema kwamba, wajumbe wanapaswa kukamilisha mazungumzo ya masuala mengine kwa miaka mitano, mkataba utakapoanza kutumika. Hii ni pamoja na majadiliano katika maeneo ya huduma-uwekezaji, manunuzi ya serikali, biashara na maendeleo, haki ya mali miliki, na sera ya ushindani. [13]

Haki ya mali miliki, na ikiwa Caribbean EPA ni mfano wowote, nchi za Afrika zinaweza kutarajia kuwa EU itawasilisha sheria mpya zinazoendelea zaidi ya viwango vya sasa vya kimataifa kama ilivyoanzishwa chini ya WTO. Watatakiwa kupitisha sheria za UPOV ambazo hutoa haki za leseni (hataza) kwa wakuzaji wa mimea (plant breeders), kuongeza faida kwa makampuni ya mbegu ya kimataifa, na labda kujiunga na UPOV. [14]

Mkataba wa kuwapa haki zaidi wawekezaji wa kigeni

Haieleweki ni umbali gani EU itaenda katika kudai huria ya uwekezaji kutoka kwa mataifa yenye nguvu kwenye sheria za Kusuluhisha Mzozo wa Mataifa (kwa kimombo Investor-State Dispute Settlement- ISDS) ambayo makampuni kutoka EU yanapata katika FTAs na Mikataba baina ya nchi za Afrika (AU). ISDS ni mfumo wa utaratibu katika mikataba ya kimataifa ya uwekezaji; inayowezesha wawekezaji kutoka nchi moja kuweza kuleta kesi dhidi ya nchi ambayo walikuwa wamewekeza, mbele ya mahakama ya usuluhishi kama wao wanaona kwamba sheria iliyowekwa katika makubaliano yao imekeukwa. Kama mazungumzo yaliyofanyika hivi karibuni yatachukuliwa kama mfano, EU inaweza kushinikiza huria zaidi iwezekanavyo pamoja na toleo lililobadilishwa la ISDS ambayo EU imeteua hivi karibuni katika mkataba wake wa biashara na Canada.

Hoja moja kubwa itakuwa ardhi. FTA inaegemea upande wa “wageni kama raia “, ambao husisitiza wageni wapewe haki sawa na wenyeji. Mataifa ya Kiafrika yasipotangaza msimamo wao, EPAs itafanya iwe hatia kwa mataifa kupinga wageni kupata na kumiliki mashamba. Zaidi ya maswala ya ardhi, sheria za kulegeza uwekezaji itahakikisha kwamba makampuni ya biashara za ukulima ya Ulaya, na makampuni ya chakula - kutoka Nestle na Danone, hadi Carrefour – watanufaika kwa kujenga na kuenea Afrika. Madhara katika sekta ya kilimo hudhuru hata zile sekta zingine, jambo ambalo ni la kushangaza kweli!

Kutokana na mipango ya biashara isiyo ya haki, sekta ya usindikaji wa chakula inaoza au inajaribu kupambana ili kukua katika nchi nyingi za Afrika. Sambamba, uwezo wa wakulima wa kuzalisha chakula kwa jamii zao na masoko ya ndani ni imeathirika na, pamoja na hayo, uhuru wa chakula. Utawala wa mazao ya biashara ya kuuza nje katika Afrika ni moja ya dalili kwamba unyonyaji wa kikoloni bado ungali hai, miaka 50-60 baada ya uhuru wa nchi nyingi za Afrika. 

Uzalishaji Na Usindikaji 

“Ikiwa mtu anajaribu kufanya mpango na wewe kulingana na mahali ulipo leo na unapopanga kwenda mahali pengine, itakuwa busara kuangalia mbele na kuhakikisha kwamba makubaliano yanatarajia mahali unakokwenda.Tatizo la EPA ni kwamba, haitarajii mahali ambapo tunataka kuwa kama uchumi wa viwanda,”
Dk. Okechukwu Enelamah, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Nigeria. [15]

Gawa ya viwanda ya Afrika ni, bila shaka, ndogo sana ambayo imesababisha Umoja wa Afrika (AU) kuzindua mpango ulioitwa, Mpango wa Hatua wa Maendeleo ya Viwanda Afrika (AIDA). AIDA ilipitishwa mwaka wa 2007. Ikiwa viwanda tayari vinakabiliwa na utata, EPA haitakuwa suluhisho ambalo Afrika inahitaji kukuza sekta yake ya viwanda.

Kulihusu suala la viwanda, utiaji wa sahihi EPA utamaanisha kuwa viwanda na bidhaa zinafaa kuzingatia kiwango cha Ulaya kabla ya kukubaliwa na soko la EU. Kama John Opoku anavyosema, kuzingatia kiwango cha Ulaya kwa kweli inamaanisha kuimarisha sekta ya viwanda vya Ulaya kutumia gharama ya Afrika. Anasema kwamba “hata kwa viwango vya kawaida vya mafuta ya mitende, lazima viwango vifikiwe kabla ya kukuruhusiwa kuuzia soko la EU. Samaki pia inapaswa kufikia kiwango fulani, vinginevyo hatuwezi kuuzia soko hilo. Kwa hivyo unaona kwamba ikawa njia ya kuzuia kapu letu la uzalishaji na kuruhusu kuendelea kuleta na kuuza bidhaa zao.” [16]

Haya yanafanyika katiba takriban mataifa yote ya Kiafrika ambayo bado huuza bidhaa ambazo malighafi na hatimaye bidhaa hizo huboreshwa huko EU na kurejea nchi ile ile kwa gharama kubwa zaidi. Kwa mfano, Kenya ni mmoja wa wazalishaji wakuu wa kahawa, lakini Mkenya wa kawaida hana uwezo wa kumudu kikombe cha kahawa. Kwa sababu hizi Tanzania na Nigeria wanateta na kukataa kuweka sahihi EPA. [17]

Malalamiko mashinani Kenya dhidi ya EPA nchini Kenya

Chama cha wakulima wadogo wa Kenya (KSSFF) na wengine wengi wanaofanya kazi ya kuhakikisha maoni ya wakulima wadogo husikilizwa au kuzingatiwa kuhusu makubaliano ya biashara. Kwa sababu hii, KSSFF pamoja na waombaji wengine sita, iliipeleka serikali ya Kenya mahakamani mwaka 2007. [18]

Kikundi hicho kilikuwa “[...] kikishtaki kutokuwepo kwa ushiriki wa umma katika mazungumzo ya EPA kwa sababu sharti ni kwamba ni lazima kuwe na ushiriki mkubwa wa umma, unaowezeshwa na serikali ya nchi. Kwa hiyo mahakama iliamua kuwa Kenya itahakikisha kuwa kuna ushiriki wa umma na serikali kuacha kupuuza na kuendelea na kujadiliana jinsi walivyotaka, “alisema Justus Lavi, mmoja wa waombaji na mwanachama wa KSSFF. [19]

Wakulima walisema kwamba rasimu ya EPA itasababisha uhaba wa chakula na kudhoofisha uhuru wa wakenya kuchagua chakula. Wao walikataa uwezekano wa madhara kwa uchumi wa Kenya kutokana na “bidhaa duni na zenye ruzuku kutoka kwa EU, na kusababisha ushindani mbaya unaweza kusababisha kufungwa kwa viwanda vya Kenya.” Wakulima walishinda kesi mwaka 2013 lakini hawakufuatilia kupata haki yao. Hata hivyo, serikali ya Kenya iliweka sahihi na kuthibitisha EPA mwaka 2016.

Ni lipi Lijalo?

Wasiwasi mwingine wa EPA ni Brexit (hili ni neno maarufu ya nia ya Uingereza kutaka kujiondoa kutoka kwa Umoja wa Ulaya) na madhara yake kwa makubaliano ya EPA. 

Si siri kwamba nchi ya Uingereza ndio mtumizi mkubwa wa bidhaa nyingi kutoka nchi hizi. Katika EAC peke yake, Uingereza ilichangia asilimia 35.5 ya jumla ya mauzo ya nje ya EAC katika EU mwaka wa 2015. Brexit inatoa wito wa dharura wa kusitishwa kwa mazungumzo hayo kwa sababu nchi zinazohusika katika haya mazungumzo zimebadilika! Afrika Kiiza kutoka SEATINI, anasema kuwa, “tunahitaji kwanza kutathmini athari za hii Brexit. [….] kwa sababu twaweza kosa kunufaika lakini EU [Uingereza ikitoka] inasimama kufaidika kwa kila njia.” [20]

Licha ya ugawaji dhahiri uliopo, EU inaendelea kushinikiza zaidi ili kambi zile kaidi kama Afrika Mashariki na Magharibi ziweze kutia sahihi kwenye makubaliano ya EPA. Haya yote yanafanyika wakati majadiliano ya Mkataba wa Cotonou, ambao utakaoisha 2020 unaendelea. Mataifa ya ACP tayari yalitangaza kwamba wanataka kubadilisha uhusiano wao na EU, wa biashara na uwekezaji kutoka biashara huru hadi iwe katika msingi bora watakaopenda, katika mkataba mpya.

Zaidi ya hayo, kuna FTA ya bara (CFTA) ambayo ilianzishwa na mkutano wa AU, lililokuwa jaribio la kufuatilia biashara ya bara zima katika ushirikiano wa Mkataba wa Abuja wa 1991. CFTA, ni jaribio la shirika la AU kujenga Jumuia la uchumi wa Afrika. Miongoni mwa vingine, CFTA itajadiliana masuala ya kuondoa ushuru, sheria ya chanzo, vikwazo visivyo vya ushuru, viwango vya usafi wa mimea na mbegu, uwezeshaji wa biashara na biashara huduma. Haya yanatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka wa 2017.

Makubaliano ya EPA inajiingiza katika kila aina ya vikwazo kama BREXIT, kuongezeka kwa mielekeo ya kitaifa na chuki dhidi ya wageni pamoja na michakato mingine ya kitaifa, ambayo huonekana maarufu zaidi kuliko mikataba ya kikanda na kimataifa. Kuna ongezeko la upinzani dhidi ya FTA katika Afrika na kwingineko. Hata ndani ya EU, kuna upinzani mkubwa wa FTA. Matokeo yake ni kuwa imekuwa vigumu kwa serikali kuweza kupitisha makubaliano haya.

Vikwazo hivi vimeleta fursa nzuri ya kufanya upinzani dhidi ya EPA na mikataba inayojiri ya FTA kama makubaliano ya Contonou. Huu ndio wakati ambapo mkataba huu wa biashara huru katika Afrika unahitaji kupingwa na miungano ya makundi inafaa kuja pamoja kushinikiza mpango mpya. Wakati ni sasa kwa nchi za Afrika kwanza kuweka mahitaji ya wananchi wao kabla kujadili na kutia sahihi FTA.  


KIAMBATISHO: Mahojiano na Justus Lavi, kutoka kwa jukwaa la wakulima wadogo wa Kenya (Kenya Small Scale Farmers Forum- KSSFF)

GRAIN: Unaeza tueleza juu ya wakati ule ulishtaki jamuhuri ya Kenya juu ya EPA?

JL: Tulishtaki jamuhuri ya Kenya juu ya EPA mwaka wa 2006. Tulikuwa tunafanya kazi na Tume ya haki za kibinadamu nchini Kenya (KHRC). Katika wakati huo, swala la EPA lilikuwa moto sana! Kabla ya kuwashtaki, Umoja wa Ulaya (EU) waliunga mkono nchi za ACP kujenga uwezo wao katika EPA. Nilikuwa mmojawapo wa wale ambao waliohudhuria mafunzo makubwa ya miezi sita huko Nakuru, Kenya. 

GRAIN: Hawakujua wanalea “mnyama”.

JL: Hawakujua ya kwamba walikuwa wanaweka makali kisu ambacho kingewakata.Tulipata mafunzo mazuri sana yaliyolipiwa na Umoja wa Ulaya katika biashara ya Kimataifa katika WTO na EPA. Wakati tulipomaliza, nilikuwa mjumbe mzuri. Nimehudhuria mikutano mingi sana Afrika, Europa na Pacific.Iliyokua ya kufana ilikuwa Cancun, Mexico, kwenye tulivua nguo na kutembea uchi kwenye ukumbi wa maskizano.Watu wa Ulaya walitoroka na mkutano ukaisha, hivyo tu! Wakati tulirudi serekali ya Kenya ilikuwa papo hapo Umoja wa Ulaya walichagua kuwakazia serikali ya Kenya kwa sababu walijua ya kwamba, kama wangepata Kenya kuweka sahihi, basi nchi zingine za Afrika Mashariki wangefuata mkondo. Tukajua ya kwamba Kenya itashikwa! KHRC iliamua kuenda kotini na nikawambia ya kwamba wakulima wataenda nao. Tukapeleka kesi yetu kotini na tukatafuta wakili mzuri. Kesi hiyo iliendelea kwa miaka mingi sana, lakini mwishowe tulishinda mwaka wa 2013.

GRAIN: Kulikuwa na wakati ambapo kampeni ilikuwa “NO EPAs”, kisha ukaanza kuzingatia na vifungu kadhaa maalum. Kwa nini? 

JL: Mchakato wa mazungumzo hauacha. EU pamoja na nchi nyingine zilizoendelea zinachukua nafasi ya mienendo ya nafasi ya soko. Kwa mfano, tunapokuwa tukizungumzia EPA, Wamarekani walitoa AGOA. Kwa kuwa mchakato huu ni wenye nguvu, kuna mabadiliko ya mara kwa mara k.m. Kuundwa kwa EU, makundi ya kikanda katika bara, kuanguka kwa Umoja wa Sovieti, wanachama wapya wa EU, kulikuwa na harakati nyingi katika EU na wakati huo, nchi za Kiafrika pia zilibadili mazungumzo. EU ilianza kurekebisha wenyewe. Kisha wachezaji wapya kama China, Japan na BRICS waliingia kwenye picha; Waliwasilisha mbadala. Tulianza kununua magari ya serikali kutoka Japan badala ya Land Rovers. Tulianza kutumia makampuni ya ujenzi wa Kichina kwa barabara zetu. EU ilianza kuboresha msimamo wao na kwa sababu mchakato wa mazungumzo ni muda mrefu sana, unapokuwa usingizi wanapozungumza kwa uzito. Kwa hiyo wakaanza kutoa kitu - lakini haya yalikuwa tu matandiko yaliyopigwa kwetu. Lakini mambo yalikuwa makubwa sana na kutupiga ngumu wakati walipopata fursa ya kusonga mkono Kenya kwa njia ya sekta ya maua. Kwa hiyo wakati Wakenya hawakuwa na uhakika wa kile walichotaka, Wazungu waliona nafasi katika biashara ya maua na hii ni sehemu ya kwa nini Kenya ililazimishwa kutia sahihi EPAs.

GRAIN: Tukimalizia, nini kilisababisha EPA kuchukua mkondo waliochukua, haswa kuhusu Kenya?

JL: Kama nilivyosema, wakati makubaliano yalipoanza, EU ilijitolea kutoa pesa kufundisha nchi za ACP kujenga uwezo wao ndio waweze kujadiliana.Ilhali nchi za EU zilikuwa zinajua kile walikuwa wanataka, nchi za ACP hawakujua kile walikuwa wapate kutoka hapo. Lakini kwa sababu ya kubadilika kwa mambo katika dunia, haswa kuanguka kwa Umoja wa Sovieti iliyoleta wanachama wapya katika EU waliokuwa hawajui juu ya EPA, huenda ya kwamba pia hao walihitaji uwezo wao kujengwa. Halafu kulikuwa na mabadiliko mengi katika Afrika na sehemu ya ACP ambayo yaliadhiri mwendo wa mahojiano. Lakini Uchina ilifanya mabadaliko makubwa, Uchina ilipeana kile Afrika haingepata mahali pengine popote.


[1] Maria Donner Abreu (2013); Preferential rules of origin in regional trade agreements. Available at https://www.wto.org/english/res_e/reser_e/ersd201305_e.pdf.

[2] GRAIN (2016); EU-ACP EPAs. Available at http://www.bilaterals.org/?-eu-acp-epas.

[3] GRAIN, (2014); Hungry for land: small farmers feed the world with less than a quarter of all farmland. Available at https://www.grain.org/article/entries/4929-hungry-for-land-small-farmers-feed-the-world-with-less-than-a-quarter-of-all-farmland

[4] Kenya Human Rights Commission; The ABC Of EAC-EU Economic Partnership Agreements (EPA). Available at http://www.khrc.or.ke/mobile-publications/economic-rights-and-social-protection-er-sp/59-the-abc-of-eac-eu-economic-partnership-agreements-epa/file.html.

[5] Kosei Fukao (2017); ChemChina completes Syngenta takeover, targets emerging markets. Available at https://asia.nikkei.com/Business/Companies/ChemChina-completes-Syngenta-takeover-targets-emerging-markets.

[6] Interview with Anne Maina.

[7] Gatonye Gathura, (2017); Kenyans consuming genetically modified foods despite import ban – study. Available at http://rocketscience.co.ke/2017/05/02/kenyans-consuming-genetically-modified-foods-despite-import-ban-study/

[8] Adapted from SEATINI (2014); EU – EAC – EPA Implementation; Maximising the opportunities and minimising the risks.

[9] Kenya Human Rights Commission; The ABC Of EAC-EU Economic Partnership Agreements (EPA). Available at http://www.khrc.or.ke/mobile-publications/economic-rights-and-social-protection-er-sp/59-the-abc-of-eac-eu-economic-partnership-agreements-epa/file.html.

[10] Business daily (2012); High cost reduces appetite for fish in the lake region. Available at http://www.businessdailyafrica.com/news/High-cost-reduces-appetite-for-fish--in-the-lake-region/539546-1640102-format-xhtml-io2vm1z/index.html

[11] Felicity Lawrence (2011); Kenyan flower industry’s taxing question. Available at https://www.theguardian.com/environment/2011/apr/01/kenya-flower-industry-tax-investigation

[12] Munyi, P., De Jonge, B., & Visser, B. Opportunities and threats to harmonization of national plant breeder’s rights legislations through regional agreements: ARIPO and SADC. African Journal of International and Comparative Law.

[13] SEATINI (2014); EU – EAC – EPA Implementation; Maximising the opportunities and minimising the risks. 

[14] GRAIN (2016); New trade deals legalise corporate theft, make farmers’ seeds illegal. Available at https://www.grain.org/e/5511

[15] Leadership Nigeria (2017); FG Taking Practical Steps To Make Economic Diversification A Reality – Enelamah. Available at http://leadership.ng/2017/06/05/fg-taking-practical-steps-make-economic-diversification-reality-enelamah/

[16] Interview with John Opoku (May, 2017). 

[17] Interview with Justus Mwololo Lavi (June, 2017). 

[18] Petition No. 1174 was filed in the High Court of Kenya under the constitutional and Human rights division. Available at http://kenyalaw.org/caselaw/cases/view/91805/.

[19] Interview with Justus Mwololo Lavi (June, 2017).

[20] Interview with Africa Kiiza (March, 2017).

 

Author: GRAIN and Kenya Food Rights Alliance (KeFRA)
Links in this article:
  • [1] https://www.grain.org/media/BAhbBlsHOgZmSSIzMjAxNy8wOC8yMS8xNF8wMl8wMV8zMjRfSGFsaV9JbGl2eW9feWFfRVBBLmpwZwY6BkVU
  • [2] https://www.grain.org/media/BAhbBlsHOgZmSSJiMjAxNy8wOC8yMS8xNF8wMl8yMF85NV9KdW11aXlhX3lhX0FmcmljYV9NYXNoYXJpa2lfRUFDX3dhX2t1ZmlraWFfc29rb19rdXRvYV9jaGluaV95YV9FUEEuanBnBjoGRVQ
  • [3] https://www.wto.org/english/res_e/reser_e/ersd201305_e.pdf
  • [4] http://www.bilaterals.org/?-eu-acp-epas
  • [5] https://www.grain.org/article/entries/4929-hungry-for-land-small-farmers-feed-the-world-with-less-than-a-quarter-of-all-farmland
  • [6] http://www.khrc.or.ke/mobile-publications/economic-rights-and-social-protection-er-sp/59-the-abc-of-eac-eu-economic-partnership-agreements-epa/file.html
  • [7] https://asia.nikkei.com/Business/Companies/ChemChina-completes-Syngenta-takeover-targets-emerging-markets
  • [8] http://rocketscience.co.ke/2017/05/02/kenyans-consuming-genetically-modified-foods-despite-import-ban-study/
  • [9] http://www.businessdailyafrica.com/news/High-cost-reduces-appetite-for-fish--in-the-lake-region/539546-1640102-format-xhtml-io2vm1z/index.html
  • [10] https://www.theguardian.com/environment/2011/apr/01/kenya-flower-industry-tax-investigation
  • [11] https://www.grain.org/e/5511
  • [12] http://leadership.ng/2017/06/05/fg-taking-practical-steps-make-economic-diversification-reality-enelamah/
  • [13] http://kenyalaw.org/caselaw/cases/view/91805/